Monday, May 28, 2012

                                                         Umri wa Lulu bado utata

                                                    Msanii wa filamu Elizabeth Michael (Lulu)           


 Msanii wa filamu Elizabeth Michael (Lulu) akiwa amezungukwa na walinzi kwenye Mahakama Kuu Dar es Salaam jana kutokana na tuhuma zinazomkabili za kuhusishwa na kifo cha msanii mwenzake Steven Kanumba

MAWAKILI wa Serikali katika kesi ya mauaji inayomkabili mwigizaji wa filamu, Elizabeth Michael ‘Lulu’, wamepinga maombi ya mawakili wa mshitakiwa huyo kutaka umri wake uchunguzwe.

Maombi hayo yalipangwa kusikilizwa jana mahakamani hapo mbele ya Jaji Fauz Twaib, lakini kabla ya kusikilizwa, mawakili wa Serikali walidai kuwa na pingamizi la kusikilizwa maombi hayo.

Awali kabla ya pingamizi hilo, mawakili wanaomtetea Lulu waliiomba Mahakama Kuu ichunguze umri wa msanii huyo au kuiamuru Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ifanye hivyo.

Lakini Wakili wa Serikali, Shadrack Kimaro aliiomba Mahakama hiyo isisikilize maombi ya Lulu kwa madai kwamba yaliwasilishwa mahakamani hapo kimakosa, huku pia sheria iliyotumika ina kasoro.

Sheria iliyotumiwa na mawakili wa utetezi ni Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009, kifungu cha 113 inayoruhusu Mahakama kufanya uchunguzi wa umri wa mshitakiwa.

Kimaro alidai kuwa maombi hayo yalikwishatolewa katika Mahakama ya Kisutu na ‘kugonga mwamba’ na kuongeza kuwa mawakili wa utetezi walitakiwa kuukatia rufaa uamuzi huo au kuomba mapitio yake, lakini si kuwasilisha maombi mapya.

Vile vile Kimaro aliyekuwa akisaidiwa na Wakili wa Serikali, Elizabeth Kaganda, alidai kuwa maombi ya pili kwa Mahakama hiyo ya kusitisha kesi ya Kisutu ni batili.

Alidai ubatili huo ni kwa sababu kesi ya Lulu Kisutu haisikilizwi, iko katika hatua ya uchunguzi na sheria inataka kesi kusimama ikiwa katika hatua ya kusikilizwa.

Hata hivyo mawakili wa Lulu, Peter Kibatala, Fulgence Masawe na Kennedy Fungamtama na Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG) Joaquine De- Melo aliyetambulishwa kama mtazamaji, walipinga.

Mawakili hao walidai kuwa waliwasilisha maombi yao mahakamani hapo kutokana na uamuzi wa Mahakama ya Kisutu uliotamka kama kuna maombi yoyote yawasilishwe katika Mahakama hiyo.

Walidai kuwa Mahakama ya Kisutu ina uwezo wa kutoa uamuzi wa maombi yao kwa mujibu wa sheria na hakuna walipokosea na kuiomba Mahakama ipuuze maombi ya mawakili wa Serikali.

Baada ya kusikiliza maombi hayo, Jaji Twaib alisema ni vema apate muda wa kutoa uamuzi kwa sababu ana safari na kupanga kutoa uamuzi huo Juni 16.

Lulu jana alionekana mchangamfu akiashiria kuanza kuzoea maisha hayo tofauti na siku za awali, alipokuwa mnyonge mahakamani na wakati mwingine akilia.

Lulu anadaiwa kufanya mauaji ya msanii mwenzake Steven Kanumba. Upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na itatajwa tena Juni 4 mwaka huu.

 

No comments:

Post a Comment