Monday, May 28, 2012

Ufugaji wa kuku ni njia ya kuondokana na umasikini

WANANCHI mkoani Mkoa mpya wa Njombe wametakiwa kukataa umasikini kwa kubuni mbinu mbalimbali ambazo zinaweza kuongeza vipato vya familia zao ikiwemo ufugaji wa kuku.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa umoja wa wanawake wilaya ya Njombe katika mkoa mpya wa Njombe, Scholastika Kevela wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani humo. Alisema kuwa, kila kaya ifuge wastani wa kuku watano kwa ajili ya mikakati ya maendeleo kutokana na ukweli kuwa bei ya kuku imeongezeka na kufikia Sh 10,000 kwa kuku moja.

Kevela alisema kuwa wakati sasa umefika kwa wananchi kuachana na dhana kuwa wao ni masikini na badala yake kuwa wabunifu ili kuweza kujiletea maendeleo kuanzia ngazi ya familia. “Wapeni kuku majina, ada, dawati, sare za shule, maendeleo na mkitaka kuku wa kula mwambieni baba atafute kuku wa nyama ndiye atakayechinjwa,” alisema kevela

Alisema kuwa, wananchi kama watafuga kuku na kuwauza kwa malengo yaliyokusudiwa hawatakuwa na shida ya kupata ada kwa ajili ya kulipia karo za watoto wao, kwani wana kuku wengi lakini hawana mipango ya jinsi kuku hao watakavyoweza kuwasaidia pindi wanapouzwa.

Pia Bi.Kevela  aliwataka wananchi hao kupanda miti ili kuwezesha Mkoa wa Njombe kuwa wa kijani. Alisema kuwa, kila nyumba iwe na miti mitano ikiwemo ya matunda ili kuweza kuhakikisha upandaji wa miti unapewa kipaumbele. Alisema kuwa, kama wananchi watazingatia kupanda miti na kuitunza basi kutakuwa na mabadiliko makubwa na Njombe itakuwa ya kijani.

Mwenyekiti huyo aliwataka viongozi wa dini kutumika kupaza sauti za watoto kwa mara nyingi wanabeba uhalisia wa mambo yanayodhihirika kuwa hawapati nafasi ya kusema.

No comments:

Post a Comment