Monday, May 28, 2012

SIASA

Shibuda: Hakuna chama kama CCM


MBUNGE wa Maswa Mashariki, John Shibuda (Chadema) ameibuka na kusema kuwa kama angekuwa na uwezo, angehakikisha kuwa chama chenye kauli za uchochezi kinashikishwa adabu na kwamba hadi sasa hajaona chama chenye nguvu mithili ya CCM.

Amekifananisha chama hicho tawala kuwa na nguvu sawa na mngurumo wa ndege ya kivita (Airforce). Alisema kuwa, mfumo wa sasa wa vyama vingi umezaa hasira kwa sababu CCM inataka kutawala, ilihali wapinzani nao wanaitaka nchi ili waitawale.

Shibuda aliyasema hayo jana, alipokuwa akitoa mada ya Demokrasia na Siasa wakati wa mafunzo elekezi ya Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya yanayoendelea hapa. Alikuwa akiwasilisha mada hiyo iliyoandaliwa na Mpango wa Kutathimini Utawala Bora Afrika (APRM).

Alisema kuwa gazeti moja la kila wiki mapema wiki hii lilikuwa na habari iliyokuwa na maneno `CCM yakaribia kuaga Ikulu’, lakini akasema kamwe hajawahi kuona chama chenye mngurumo wa Airforce kuweza kuizidi CCM na kushika nchi.

“Ningekuwa na uwezo mara ninaposikia kuna uchochezi sitamkamata mtu aliyetoa maneno ya uchochezi, bali nitakipiga faini chama chake kwa lengo la kuhakikisha kuwa kinabadili lugha zake, kwani chama chenye uchochezi kikipigwa faini mara nyingi kitakuwa na nguvu tena?” alihoji Shibuda.

Alisema kuwa, fitna mara nyingi zimekuwa malighafi za kisiasa kutokana na maneno matamu, lakini APRM ni chujio na kuwa mfumo wa vyama vingi huzaa wawindaji.

“Kiongozi anayekaa ofisini hawezi kujua kiu ya wananchi wake, ni lazima kujisahihisha na kujitathimini, kwani Serikali na siasa ni kama mapacha, lakini cha muhimu ni kujiuliza vipi tutalinda mitaji yetu? Kwani kuna vishawishi vya kuacha mema na kukumbatia upumbavu, lakini matunda matamu hutambulishwa na mbegu za kuzaa matunda matamu,” alisema.

Aliongeza kuwa, siasa za sasa zimejaa unafiki mfano wa malezi ya machokoraa (watoto wasio na makazi maalumu) ambayo hayakupata malezi ya baba na mama.

“Mfumo wa vyama vingi unazaa hasira kwa sababu tunataka kuwakomoa wapinzani na CCM inasema inataka kuwamaliza wapinzani, lakini ukimaliza mazalia ya mbu malaria haitakuwepo,” alisema.

Alisema kuwa, Rais Jakaya Kikwete ni mwanasiasa na bila siasa hakuna kilainishi cha kuongoza na kutawala .

“Wakoloni walitumia machifu wa Kisukuma kutawala, wanaweza kukushangilia ukajua wanafurahia kumbe wanatafuta mwanya wa kukuadhibu,” alisema Shibuda. Alisema kuwa mwanzoni alikuwa CCM na sasa yuko upinzani, hivyo ana taswira ya nchi inakoelekea.

Aliongeza: “Najiuliza, naacha urithi gani kwa wadogo zangu waliochaguliwa kuwa Wakuu wa Wilaya?”.

Shibuda aliwataka viongozi wa Serikali kuhakikisha wanatunza vizuri historia ya nchi akisisitiza historia inahifadhiwa, lakini kama mtoto ni chokoraa, hatakuwa na uwezo wa kutunza historia.

Aliongeza kuwa, siasa ni daraja la maoni kwa ajili ya kuongoza umma na kila chama kimekuwa kikishindana kwa lengo la kuhakikisha kuwa kinashinda uongozi.

Aidha, Shibuda alitumia fursa hiyo kukishukuru CCM kutokana na uelewa wake, huku akisema hataki chama hicho kife, kama ambavyo pia hataki Chadema ife.

Mafunzo hayo elekezi yanayofanyika mjini Dodoma yanahudhuriwa na Wakuu wa Mikoa 24, Makatibu Tawala wa Mikoa 25 na Wakuu wa Wilaya 133.

No comments:

Post a Comment