Tuesday, June 12, 2012

                         Ziara za Pinda zazua balaa bungeni                                                     Waziri Mkuu,Mizengo Pinda
MBUNGE wa Viti Maalumu (Chadema), Rose Kamili ameibua tuhuma nzito dhidi ya Ofisi ya Waziri Mkuu, akisema mtendaji mmoja wa Serikali alikamatwa kutokana na kushindwa kukusanya mchango wa mbuzi tisa za zawadi kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wakati wa ziara yake Wilaya ya Maswa, mkoani Simiyu.

Kamili alirusha kombora hilo, wakati akiuliza swali la nyongeza kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Aggrey Mwanri baada ya swali la msingi lililoulizwa na Mbunge wa Maswa Mashariki, Sylvester Kasulumbayi (Chadema), kuhusu mipaka ya madaraka kati ya Serikali za Mitaa na Serikali Kuu inaanzia na kuishia wapi kiutendaji.

Baada ya swali hilo la msingi, Kamili aliuliza swali la nyongeza akisema Mkuu wa Wilaya ya Maswa aliwaagiza watendaji wote wa kata kukusanya mbuzi ikiwa ni zawadi za ujio wa Waziri Mkuu katika wilaya yao walioshindwa walikamatwa.

Akijibu swali hilo, Mwanri alisema ofisi yake haina taarifa ya tuhuma hizo na kumtaka mbunge huyo azithibitishe. Alisema Serikali haina utaratibu wa kuomba kupewa zawadi mbalimbali kwa viongozi wake na kama mbunge huyo ana ushahidi wa suala hilo autoe.

Mara baada ya majibu hayo, Spika wa Bunge, Anne Makinda alimpa fursa mbunge huyo kueleza kama anao ushahidi huo na akajibu kuwa anao kwani aliona hata kupitia luninga Waziri Mkuu Pinda akikabidhiwa zawadi.

Hata hivyo, majibu hayo ya Kamili  yalionekana kutomridhisha Spika Makinda ambaye alisema taarifa za luninga haziwezi kuwa ushahidi na akawataka wabunge kuwa makini na taarifa wanazotoa bungeni.
Awali, Kamili aliulizia juu ya operesheni ya kuhamisha wakazi wa pori la Maswa ambao nyumba zao kadhaa zilichomwa moto na wafugaji kadhaa kutimuliwa bila kujua pa kwenda.

Akijibu swali hiyo, Mwanri alisema mgogoro huo wa kuhamishwa wananchi hao, tayari ulifuatiliwa na Serikali na Waziri wa Nchi, Tamisemi wakati huo, George Mkuchika alikwenda katika eneo hilo na kuzungumza na wananchi na kupata taarifa sahihi.

Hata hivyo, alisema wananchi wa vijiji saba vya eneo hilo, walikubaliana kuanzisha Hifadhi ya Jamii (WMA) na kutoa eneo hilo kwa mwekezaji jambo ambalo lilitekelezwa.

Awali, akijibu swali la Kasulumbayi, Naibu Waziri Mwanry alisema wakuu wa mikoa na wilaya nchini, hawaruhusiwi kwa mujibu wa sheria, kuingilia utendaji kazi wa mamlaka za Serikali za Mitaa, ikiwa zinatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sera, sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa na Serikali.


Kasulumbayi alitaka kujua inakuwaje wakuu wa mikoa na wilaya ambao kiutendaji ni watumishi wa Serikali Kuu, wanatoa amri kwa watendaji walio chini ya wakurugenzi wa wilaya, kuhamisha wananchi katika maeneo yao. Akahoji mpaka wa madaraka kati ya Serikali za Mitaa na Serikali Kuu unaanzia na kuishia wapi kiutendaji?

Mwanri alisema mkuu wa mkoa kwa mujibu wa Sheria ya Tawala za Mikoa Na.19 ya mwaka 1997, katika vifungu Na 5, 6 na 7 ana wajibu wa kusimamia kazi na shughuli zote za Serikali katika mkoa ikiwa  ni pamoja na kuziwezesha mamlaka za Serikali za Mitaa, kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizotungwa na Bunge.

Alisema majukumu ya wakuu wa wilaya yametengwa katika kifungu Na.14 (1-3) cha Sheria ya Tamisemi, Na.19 ya mwaka 1997 kwamba yeye ndiye msimamizi mkuu wa shughuli za Serikali katika wilaya yake.

“Hivyo madaraka ya jumla ya mkuu wa wilaya yanatiririshwa kutoka kwa Mheshimiwa Rais kupitia kwa mkuu wa mkoa, kwa upande wa watendaji walio chini ya mkurugenzi wa halmashauri, wao ni watekelezaji wa shughuli za Serikali kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo,” alisema.

Hata hivyo, alisema mipaka ya madaraka kati ya Serikali za Mitaa na Serikali Kuu imeanishwa katika Sheria za Mamlaka za Serikali za Mitaa na Sheria ya Tawala za Mikoa Na 19 ya 1997.

“Kwa kuzingatia sheria hizo ni kwamba mkuu wa mkoa na wilaya anaruhusiwa kuingilia kati inapotokea mamlaka za Serikali za Mitaa zimeshindwa kutekeleza majukumu yao au kukiuka misingi ya sera na sheria zilizopo.

No comments:

Post a Comment