Tuesday, June 5, 2012

                                             Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa

 

Kawambwa kutangaza majina 100 wanaodhaminiwa MCL 

WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa leo anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya kutangaza majina 100 ya wanafunzi watakaopata udhamini wa elimu.

Udhamini huo unatolewa chini ya mpango maalum wa kusaidia ukuaji wa elimu unaoendeshwa na Mwananchi Communications Limited (MCL) kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne.

MCL ndiyo inayochapisha magazeti ya mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti.
Ofisa Masoko wa MCL, Edward Uisso alisema jana kuwa mara baada ya Waziri  kuyatangaza majina hayo   yatachapishwa katika magazeti yote ya MCL kesho.

Uisso alisema mpango huo uliopewa jina la “Paa na Mwananchi” ulihusisha  watoto wa Kitanzania tu wanaosoma shule za umma kote nchini na utaanza mara moja kwa washindi waliochaguliwa.

“Harakati za ‘Paa na Mwananchi’ zinafikia mwisho baada ya kuanza  Aprili 2, mwaka huu na leo washindi watatangazwa ambao kesho majina yao yatachapishwa katika magazeti yote ya MCL,” alisema Uisso na kuongeza:

Mpango huu wa Paa na Mwananchi unafanyika katika nchi zote za Afrika Mashariki ambazo Kampuni ya Nation Media Group (NMG), ina matawi, huu ni mpango wa kutoa udhamini wa elimu kwa wananchi wote ambao hawana uwezo wa kusomesha watoto wao.

Uisso alisema udhamini huu utahusu karo yote ya shule, sare kwa mwanafunzi, vitabu, madaftari na mahitaji mengine muhimu ya mwanafunzi.

Watoto watakaopata ufadhili huu, kuna wakati watakuwa wanafanya ziara ya kimasomo  katika nchi za Afrika Mashariki, lengo likiwa ni kupata uelewa tofauti na kubadilisha mawazo na wenzao.

Uisso alisema kuwakutanisha na wenzao wa nchi za Afrika Mashariki ni  kuwajenga watoto kifikra ili waweze kuwa na uwezo wa kushindana na wenzao kutoka nchi za husika na nje ya ukanda huu.

“Katika ziara kutakuwa na wataalamu waliobobea katika taaluma mbalimbali watakaowapa mafunzo wanafunzi hao na wakati mwingine wataalamu hao watakuja hapa nchini kuwafundisha wakiwa hapa hapa,” alisema Uisso.

No comments:

Post a Comment