Monday, June 18, 2012

MWAKALEBELA AKUNWA NA UJUMBE WA NAPE

 
NA mcdonald masse-Iringa
ALIYEKUWA mshindi wa kura za maoni ndani ya chama cha mapinduzi (CCM) katika kinyang'anyiro cha kumsaka mgombea ubunge wa CCM jimbo la Iringa mjini mwaka 2010 Frederick Mwakalebela ameeleza kufurahishwa na kauli ya katibu wa itikadi na uenezi wa CCM Taifa Nape Nnauye kuhusu ukweli wa mbunge Mchungaji Peter Msigwa (CHADEMA) kupita katika uchaguzi huo.

Hivyo awataka vijana wa kuacha kukimbilia vyama vya upinzani na badala yake kuendelea kutulia ndani ya CCM kwa madai kuwa kuna mikakati kambambe anayoifanya kwa ajili ya kuwawezesha vijana hao ili kuwa wajasiriamali badala ya kushinda vijiweni .
Alisema kuwa kuwa uwazi na ukweli wa Nape kuhusu makosa yaliyojitokeza katika jimbo hilo la Iringa mjini ni moja kati ya mambo ambayo wananchi wa jimbo la Iringa mjini walitegemea kuelezwa na kiongozi huyo .

Hivyo alisema kuwa mbali ya kuwa bado hajaamua kugombea ama kutogombea katika jimbo hilo ila bado ataendelea kuwa kada mzuri wa CCM na wala hatajaribu kukihama chama chake CCM kama ambavyo baadhi ya makada wenzake wanavyofanya.

" Napenda kumpongeza sana katibu wangu wa itikadi na uenezi Taifa Nape Nnauye kwa kuwaeleza ukweli wapiga kura wa jimbo la Iringa mjini ambao baadhi yao walikuwa wakirubuniwa na vyama vya upinzani kuwa labda CCM haitaweka ukweli wa kasoro zilizojitokeza katika uchaguzi mkuu mwaka 2010.....nataka vijana wa jimbo la Iringa mjini watambue kuwa mimi bado ni mwana CCM na nitaendelea kuwa karibu na chama changu"

Mwakalebela alitoa kauli hiyo leo alipozungumza na mtandao huu wa www.francisgodwin.blogspot.com kwa njia ya simu kuhusiana na msimamo wake kisiasa na maoni yake juu ya vijana wanaoendelea kushabikia upinzani kama njia ya kuchukizwa na hatua ya CCM mwaka 2010 kuengua jina la Mwakalebela.

Alisema kuwa ni vema vijana kutambua kuwa CCM ndicho chama chenye mwelekeo wa kuwatumikia wananchi na kuwa ni vema vijana hao kuendelea kubanana ndani ya CCM badala ya kuhama chama hicho.

Akielezea kuhusu mikakati yake ya kuwasaidia vijana wa jimbo hilo la Iringa mjini Mwakalebela alisema kuwa bado anauchungu na vijana wa Iringa mjini na hivyo amejipanga kuwasaidia kuwaunganisha na vikundi vya ujasiria mali pamoja na kuendelea kuwaunganisha vijana hao bila kujali itikadi ya kisiasa katika michezo ambayo itaanza hivi karibuni.

Kwa upande wake baadhi ya vijana na wazee wa mjini Iringa wamepongeza ziara hiyo ya Nape mjini Iringa kuwa ni ziara iliyolenga kumaliza uongo wa uongozi wa viongozi wa Chama cha Demokrasia na maendeleo (Chadema) dhidi ya serikali ya CCM .

Alisema mzee Ambweni Kyando mkazi wa Mwangata katika Manispaa ya Iringa kuwa bado anashangazwa na baadhi ya waliokuwa wagombea katuka kura za maoni ubunge jimbo la Iringa mjini akiwemo Zuberi Mwachura kukimbilia upinzani wakati ni mmoja kati ya makada wazuri wa CCM waliotegemewa kuja kupewa nafasi za juu

Wednesday, June 13, 2012

                           Dk Mwakyembe awasha moto TRL



BAADA ya kusafiri kwa treni kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma, Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amebaini hujuma nzito katika Shirika la Reli Tanzania (TRL) ikiwamo ofisa mmoja kuwaibia abiria kwa kughushi viwango vya nauli na ameagiza afukuzwe kazi.

Licha ya kuagiza kutimuliwa kwa ofisa huyo, pia alitangaza kuandaliwa utaratibu wa kufanya mabadiliko kadhaa katika kuboresha usafiri huo, ikiwamo kuondoa malipo ya nusu nauli kwa watoto wadogo kuanzia miaka mitatu hadi miaka 10 na pia kuondolewa kwa utaratibu wa malipo ya mizigo midogo ya abiria.

Juzi, Dk Mwakyembe ambaye tayari amewang’oa vigogo wanne wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), aliamua kusafiri kwa treni hadi Dodoma akitokea Dar es Salaam ili kujionea utendaji kazi wa shirika hilo.

Mara baada ya kuwasili katika Stesheni ya Dodoma saa 1:30 asubuhi, Waziri Mwakyembe alizungumza na waandishi wa habari na kusema akiwa katika safari hiyo, amepata fursa za kutembelea mabehewa yote na kuzungumza na abiria.

Dk Mwayembe alisema ingawa safari ilikuwa nzuri, kuna mengi ambayo ameyabaini ambayo ni pamoja na abiria kulipa nauli kubwa na kuandikiwa tiketi tofauti jambo ambalo alisema ni wizi na kamwe wizara yake haiwezi kulifumbia macho.

“Unakuta nauli halali ni Sh9,000 lakini, abiria ameandikiwa Sh29,000. Sasa nimeagiza huyu anayehusika afuatiliwe na kujulikana na nipewe taarifa ameondolewa,” aliagiza Dk Mwakyembe.
Alisema pia katika safari hiyo, alibaini uchakavu mkubwa wa mabehewa na hakuna tofauti ya daraja la tatu na la kwanza, upungufu mwingine ni katika utendaji na taratibu jambo ambalo linapaswa kuchukuliwa hatua.

Dk Mwakyembe alisema si vyema mtoto kuanzia miaka mitatu kulipishwa nusu nauli, kwani taratibu zinapaswa kufanywa ili hadi mtoto wa miaka 10 ikiwezekana asilipishwe nauli kwani treni ndiyo usafiri wa umma.

Kuhusu mizigo, alisema kwa sasa mizigo ya abiria inalipiwa kwa kilo kama ilivyo usafiri wa ndege jambo ambalo si sawa kwani mzigo wa abiria kuanzia kilo 20 unalipishwa jambo ambalo linapaswa kuangaliwa.

“Usafiri huu mimi nasema ndiyo wa umma hivyo, tusizuie watu kupeleka hata zawadi nyumbani kwao ni vyema tuwe na utaratibu walau mizigo kidogo ya abiria isilipiwe,” alisema Dk Mwakyembe.

Safari tatu kwa wiki
Akizungumzia tatizo la ratiba za usafiri, Dk Mwakyembe alisema mipango inafanywa ili kufikia Desemba, mwaka huu walau kuwe na safari tatu za kutoka Dar es Salaam hadi  Kigoma na Tabora na kuondoa kero zilizopo sasa.

Waziri huyo alisema anaamini safari hizo zikirejea, zitapunguza wingi wa abiria na msongamano wa watu kwenye treni na pia zitasaidia kuanza kwa usafirishaji wa mizigo kwa kutumia usafiri huo.
“Tutawaomba wabunge wapitishe bajeti yetu na wapande treni ili kuona usafiri huu, nina amani tukiondoa upungufu kidogo, huu utakuwa usafiri mzuri sana,” alisema.

Hujuma
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tzeba ambaye allimpokea Dk Mwakyembe alisema licha ya kuwepo hujuma katika nauli za abiria, pia wamebaini hujuma kubwa katika mizigo inayosafirishwa kwa reli katika mashirika yote ya TRC na Shirika la Tanzania na Zambia (Tazara).

Alisema maofisa wasio waadilifu wa mashirika hayo, wamekuwa wakisafirisha mizigo mingi lakini inayoandikiwa na kulipwa serikalini ni ile yenye uzito mdogo.

“Utakuta mzigo wa tani 40 hadi 60 unaandikiwa tani 10 au 20 fedha nyingine zinaingia mifukoni mwa wajanja, hatutakubali jambo hili,” alisema Dk Tzeba
Alisema yeye na waziri wake, pamoja na maofisa wengine, watakuwa wakisafiri kwa kushtukiza kwa reli mara kwa mara ili kubaini hujuma zote na kuwachukulia hatua wahusika mara moja.
“Mimi nilikuja hapa Dodoma kwa kiberenge na baadhi ya wabunge wa kamati ya miundombinu na leo amekuja waziri kwa treni hii haitakuwa mara yetu ya kwanza, tutasafiri sana kwa reli ili kubaini hujuma zilizopo,” alisema Dk Tzeba.

Tuesday, June 12, 2012

Tegete: Yanga imelamba dume kumsajili Yondani 


Tegete

 


MSHAMBULIAJI wa Yanga, Jerryson Tagete amesema kusajiliwa klabu hiyo ya Jangwani beki wa zamani wa Simba, Kelvin Yondan kutasaidia kufika mbali katika mashindano ya ndani na nje kutokana na uwezo mkubwa aliona mlinzi huyo.
Tegete aliyeongeza mkataba wa miaka miwili zaidi kuicheza Yanga, alisema ana imani kubwa na uwezo wa Yondani na kwamba uongozi wa Yanga hakufanya chaguo baya kumsajili.
 Mpachika mabao huyo wa Jangwani aliyepwaya msimu uliomalizika, amesema eye binafsi anafurahi kubaki Yanga na atakuwa tayari kuonyesha ushirikiano na beki wao mpya Yondani.
Akizungumza jana na kituo kimoja cha Radio, Tegete alisema kinachomfurahisha zaidi ni uwapo wa Yondani kwenye kikosi hicho kilichopoteza mwelekeo msimu uliopita na kumaliza ligi nafasi ya tatu ikiwa ni mara ya kwanza katika kipindi cha zaidi ya miaka 20.
"Tathimini yangu ni kwamba, Yondani ni beki mzuri anayekubalika na wengi. Kweli nafarijika kuja kwake Jangwani nikiamini atakuwa msaada mkubwa," alisema Tegete aliyewahi kuhusishwa kutaka kuhamia Simba msimu ujao.
Kuhusu kuongezewa mkataba, Tegete alisema amefurahishwa na hatua ya viongozi wake kwa vile ana mapenzi ya dhati na klabu hiyo ya Jangwani, mabingwa wa sas Kombe la Kagame.
"Sikuwahi kuwa na mpango wa kuhama Yanga, lakini naweza kufanya hivyo iwapo tu nitapata klabu ya kucheza nchi ya Tanzania na siyo kinyume chake," alisema.
Wakati huohuo, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amewataka viongozi wa Yanga na Simba kutoendelea na utamaduni wa kupoteza muda kwa mambo yaliyokosa mashiko.
Kauli hiyo ametoa jana baada ya kuwepo na mvutano kati ya viongozi wa timu hizo mbili juu ya usajili wa beki wa Simba Kevin Yondani ambaye inadaiwa kuwa amesajiliwa na Yanga.
Alisema viongozi wa timu hizo mbili wote wanazifahamu taratibu za usajili hivyo kama kuna udanganyifu kila kitu kipo wazi hivyo wasipoteza muda kwa mambo yasiyokuwa ya msingi.
"Lazima kati ya pende hizo mbili kutakuwepo na mmoja ambaye ni muongo hivyo hakuna haja ya kupoteza muda wa kupigizana kelele kwa sababu kila kitu kipo wazi" alisema Tenga.

                         Ziara za Pinda zazua balaa bungeni



                                                     Waziri Mkuu,Mizengo Pinda
MBUNGE wa Viti Maalumu (Chadema), Rose Kamili ameibua tuhuma nzito dhidi ya Ofisi ya Waziri Mkuu, akisema mtendaji mmoja wa Serikali alikamatwa kutokana na kushindwa kukusanya mchango wa mbuzi tisa za zawadi kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wakati wa ziara yake Wilaya ya Maswa, mkoani Simiyu.

Kamili alirusha kombora hilo, wakati akiuliza swali la nyongeza kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Aggrey Mwanri baada ya swali la msingi lililoulizwa na Mbunge wa Maswa Mashariki, Sylvester Kasulumbayi (Chadema), kuhusu mipaka ya madaraka kati ya Serikali za Mitaa na Serikali Kuu inaanzia na kuishia wapi kiutendaji.

Baada ya swali hilo la msingi, Kamili aliuliza swali la nyongeza akisema Mkuu wa Wilaya ya Maswa aliwaagiza watendaji wote wa kata kukusanya mbuzi ikiwa ni zawadi za ujio wa Waziri Mkuu katika wilaya yao walioshindwa walikamatwa.

Akijibu swali hilo, Mwanri alisema ofisi yake haina taarifa ya tuhuma hizo na kumtaka mbunge huyo azithibitishe. Alisema Serikali haina utaratibu wa kuomba kupewa zawadi mbalimbali kwa viongozi wake na kama mbunge huyo ana ushahidi wa suala hilo autoe.

Mara baada ya majibu hayo, Spika wa Bunge, Anne Makinda alimpa fursa mbunge huyo kueleza kama anao ushahidi huo na akajibu kuwa anao kwani aliona hata kupitia luninga Waziri Mkuu Pinda akikabidhiwa zawadi.

Hata hivyo, majibu hayo ya Kamili  yalionekana kutomridhisha Spika Makinda ambaye alisema taarifa za luninga haziwezi kuwa ushahidi na akawataka wabunge kuwa makini na taarifa wanazotoa bungeni.
Awali, Kamili aliulizia juu ya operesheni ya kuhamisha wakazi wa pori la Maswa ambao nyumba zao kadhaa zilichomwa moto na wafugaji kadhaa kutimuliwa bila kujua pa kwenda.

Akijibu swali hiyo, Mwanri alisema mgogoro huo wa kuhamishwa wananchi hao, tayari ulifuatiliwa na Serikali na Waziri wa Nchi, Tamisemi wakati huo, George Mkuchika alikwenda katika eneo hilo na kuzungumza na wananchi na kupata taarifa sahihi.

Hata hivyo, alisema wananchi wa vijiji saba vya eneo hilo, walikubaliana kuanzisha Hifadhi ya Jamii (WMA) na kutoa eneo hilo kwa mwekezaji jambo ambalo lilitekelezwa.

Awali, akijibu swali la Kasulumbayi, Naibu Waziri Mwanry alisema wakuu wa mikoa na wilaya nchini, hawaruhusiwi kwa mujibu wa sheria, kuingilia utendaji kazi wa mamlaka za Serikali za Mitaa, ikiwa zinatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sera, sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa na Serikali.


Kasulumbayi alitaka kujua inakuwaje wakuu wa mikoa na wilaya ambao kiutendaji ni watumishi wa Serikali Kuu, wanatoa amri kwa watendaji walio chini ya wakurugenzi wa wilaya, kuhamisha wananchi katika maeneo yao. Akahoji mpaka wa madaraka kati ya Serikali za Mitaa na Serikali Kuu unaanzia na kuishia wapi kiutendaji?

Mwanri alisema mkuu wa mkoa kwa mujibu wa Sheria ya Tawala za Mikoa Na.19 ya mwaka 1997, katika vifungu Na 5, 6 na 7 ana wajibu wa kusimamia kazi na shughuli zote za Serikali katika mkoa ikiwa  ni pamoja na kuziwezesha mamlaka za Serikali za Mitaa, kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizotungwa na Bunge.

Alisema majukumu ya wakuu wa wilaya yametengwa katika kifungu Na.14 (1-3) cha Sheria ya Tamisemi, Na.19 ya mwaka 1997 kwamba yeye ndiye msimamizi mkuu wa shughuli za Serikali katika wilaya yake.

“Hivyo madaraka ya jumla ya mkuu wa wilaya yanatiririshwa kutoka kwa Mheshimiwa Rais kupitia kwa mkuu wa mkoa, kwa upande wa watendaji walio chini ya mkurugenzi wa halmashauri, wao ni watekelezaji wa shughuli za Serikali kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo,” alisema.

Hata hivyo, alisema mipaka ya madaraka kati ya Serikali za Mitaa na Serikali Kuu imeanishwa katika Sheria za Mamlaka za Serikali za Mitaa na Sheria ya Tawala za Mikoa Na 19 ya 1997.

“Kwa kuzingatia sheria hizo ni kwamba mkuu wa mkoa na wilaya anaruhusiwa kuingilia kati inapotokea mamlaka za Serikali za Mitaa zimeshindwa kutekeleza majukumu yao au kukiuka misingi ya sera na sheria zilizopo.

Thursday, June 7, 2012

KAA TAYARI KWA UJIO WA KITUO KIPYA CHA REDIO KATIKA MJI WA MAKAMBAKO NDANI YA MKOA MPYA WA NJOMBE.

Tuesday, June 5, 2012





                                             Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa

 

Kawambwa kutangaza majina 100 wanaodhaminiwa MCL 

WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa leo anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya kutangaza majina 100 ya wanafunzi watakaopata udhamini wa elimu.

Udhamini huo unatolewa chini ya mpango maalum wa kusaidia ukuaji wa elimu unaoendeshwa na Mwananchi Communications Limited (MCL) kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne.

MCL ndiyo inayochapisha magazeti ya mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti.
Ofisa Masoko wa MCL, Edward Uisso alisema jana kuwa mara baada ya Waziri  kuyatangaza majina hayo   yatachapishwa katika magazeti yote ya MCL kesho.

Uisso alisema mpango huo uliopewa jina la “Paa na Mwananchi” ulihusisha  watoto wa Kitanzania tu wanaosoma shule za umma kote nchini na utaanza mara moja kwa washindi waliochaguliwa.

“Harakati za ‘Paa na Mwananchi’ zinafikia mwisho baada ya kuanza  Aprili 2, mwaka huu na leo washindi watatangazwa ambao kesho majina yao yatachapishwa katika magazeti yote ya MCL,” alisema Uisso na kuongeza:

Mpango huu wa Paa na Mwananchi unafanyika katika nchi zote za Afrika Mashariki ambazo Kampuni ya Nation Media Group (NMG), ina matawi, huu ni mpango wa kutoa udhamini wa elimu kwa wananchi wote ambao hawana uwezo wa kusomesha watoto wao.

Uisso alisema udhamini huu utahusu karo yote ya shule, sare kwa mwanafunzi, vitabu, madaftari na mahitaji mengine muhimu ya mwanafunzi.

Watoto watakaopata ufadhili huu, kuna wakati watakuwa wanafanya ziara ya kimasomo  katika nchi za Afrika Mashariki, lengo likiwa ni kupata uelewa tofauti na kubadilisha mawazo na wenzao.

Uisso alisema kuwakutanisha na wenzao wa nchi za Afrika Mashariki ni  kuwajenga watoto kifikra ili waweze kuwa na uwezo wa kushindana na wenzao kutoka nchi za husika na nje ya ukanda huu.

“Katika ziara kutakuwa na wataalamu waliobobea katika taaluma mbalimbali watakaowapa mafunzo wanafunzi hao na wakati mwingine wataalamu hao watakuja hapa nchini kuwafundisha wakiwa hapa hapa,” alisema Uisso.

Friday, June 1, 2012




Wasanii maarufu wa Orijino Komedi na msanii wa muziki wa kizazi kipya, Judith Wambura ‘Lady Jay Dee’ na bendi yake ya Machozi wanatarajiwa kutumika kutunisha mfuko utakaofanikisha Siku ya Utalii Duniani, ambayo kitaifa itafanyika mkoani hapa. Zaidi ya Sh milioni 120 zimekadiriwa kutumika kwa ajili ya maadhimisho ya sherehe hiyo itakayofanyika kwa wiki nzima kuanzia Septemba 28 hadi Oktoba 4, mwaka huu.

Mratibu wa Kamati ya Maandalizi ya Sherehe hizo, Fidiah Nakamendu alisema jana kwenye kikao cha maandalizi kwamba sherehe hizo zitafanyika nje kidogo ya Manispaa ya Iringa katika Kijiji cha Nduli, karibu na Uwanja wa Ndege wa Nduli. Alisema wasanii hao watafanya maonyesho yao katika mabonanza yatakayoandaliwa baadaye mjini Iringa. Alitaja mikakati mingine itakayofanikisha upatikanaji wa fedha hizo kuwa ni pamoja na kutuma barua za maombi ya michango kwa wadau mbalimbali wa utalii kama asasi za kiserikali na zisizo za kiserikali.

Mikakati mingine ni pamoja na kuandaa chakula cha hisani na kufanya tamasha la kitamaduni la chakula, mavazi na ngoma za asili. Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Mrisho ambaye ni Mwenyekiti wa sherehe hizo, ameagiza kamati hiyo ifungue akaunti maalumu ya sherehe itakayokuwa na wajumbe wawili kutoka sekta ya umma na wengine wawili kutoka sekta binafsi na kuupongeza uamuzi wa kamati kufanyia sherehe hizo karibu na Uwanja wa Ndege wa Nduli kwani utaongeza changamoto katika kuendeleza utalii wa Mkoa wa Iringa. Kulingana na waandaaji, wakati wa sherehe hizo wageni watapata fursa ya kutembelea vivutio mbalimbali vilivyopo mkoani hapa kwa gharama nafuu, pia kutakuwa na maonyesho ya vikundi mbalimbali vya burudani.